Na Haji Nassor, Pemba
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi, ameiagiza kampuni ya MECCO inayojenga barabara ya Wete-Gando na Wete-Konde, kufanya kila juhudi kuhakikisha kazi hiyo ilioanza tena, haisiti hadi pale watakapoikabidhi barabara hizo kwa serikali.
Alisema wananchi wanaotumia barabara hizo wameshachoshwa na ahadi zisizotekelezwa, hivyo ni vyema kwa sasa wakafanya kila njia kuhakikisha wanazimalizia kwa kiwango cha lami.
Alitoa agizo hilo siku chache baada ya kampuni hiyo kuingiziwa fedha zaidi ya shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa barabara hizo.
Alisema kwa sasa hakuna sababu tena kwa kampuni hiyo kuingia mitini, kwa vile serikali kwa kushirikiana na washirika wake wa maendeleo ukiwemi mfuko wa Sudia Fund, kutoa fedha.
Alisema wananchi wa maeneo hayo wanachotaka sasa ni kutumia barabara hizo katika hali ya usalama kwa vipindi vyote, sambamba na kuimarisha harakati zao za uchumi.
“Mimi niinasihi kampuni ya MECCO wajitahidi sana kujenge barabara hiyo kwa mwendo wa kasi, ili wananchi waanze kuzitumia barabara zao,” alisema.
Akizungumzia hilo Ofisi Mdhamini wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Ahmed Baucha, alikiri kwamba kampuni ya MECCO imeanza kazi tena ya ujenzi wa barabara hizo, ambapo kwa sasa wameanzia na barabara ya Wete-Gando.
Kwa mara ya kwanza barabara hizo zilianza kujengwa mwaka 2009 lakini ujenzi ulisitishwa kutokana na serikali na washirika wake wa maendeleo (AfDB) na Mfuko wa Sudia, kutoingiza fedha kwa wakati.