Na Mwandishi wetu
SHIRIKA LA Umeme Zanzibar (ZECO) limesema kukatika umeme katika maeneo yote ya Unguja na Pemba, kulitokana na kuzimika ghafla mitambo ya kuzalisha umeme Tanzania Bara.
Taarifa ya ZECO kwa vyombo, ilisema kuzimika kwa mitambo hiyo kulisababisha kuondoka kwa gridi ya taifa ambayo Zanzibar inapata umeme kupitia gridi hiyo.
Kutokana na tatizo hilo maeneo yote ya Unguja na Pemba na baadhi ya mikoa mingi ya Tanzania Bara yalikosa umeme.
Wakati akizungumza na kituo kimoja cha habari nchini ,Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Felchesim Mramba, alisema chanzo hasa kilichopelekea kuzimika kwa mitambo hiyo bado hakijajulikana na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.
ZECO limeelezea kusikitishwa na kukatika kwa umeme huko kwani shughuli nyingi za kimaendeleo zilisimama ikiwemo wananchi kukosa kutazama na kusikiliza maelezo ya moja kwa moja kutoka Baraza la Wawakilishi, kuangalia fainali za Kombe la Dunia na kusimama kwa shughuli nyengine za kimaendeleo.
Taarifa hiyo imesema Shirika litaendelea kutoa taarifa za kina kwa vyanzo vyovyote vile vya kukatika kwa umeme na kuwaomba wananchi kuwa wastahamilivu wakati wa matukio kama hayo yanapotokea.
Aidha taarifa hiyo imewataka wananchi kuacha vitendo vya kuhujumu miundombinu kwa kuchimba mchanga chini ya njia za umeme.