Na Said Ameir,Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein, amempelekea salamu za pongezi Rais wa India, Shri Pranab Mukherjee kwa kutimiza miaka 68 ya uhuru wa nchi hiyo.
“Inanipa furaha kutumia fursa hii adhimu kukutumia wewe binafsi Rais na kupitia kwako kwa wananchi wa India salamu za pongezi kutoka kwangu na kutoka kwa wananchi wa Zanzibar kwa kusherehekea miaka 68 ya uhuru wa nchi yenu ,” salamu hizo zimeeleza.
Katika salamu hizo Dk. Shein amebainisha kuwa wananchi wa Zanzibar wanajivunia uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yao na wananchi wa India na kwamba azma yao ni kuona uhusiano na ushirikiano huo unazidi kuimarika siku hadi siku.
Aliongeza kuwa wananchi wa Zanzibar wanafarijika kuona India imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika kipindi cha miaka 68 ya uhuru wake na kwamba maendeleo hayo yamekuwa yakiwanufaisha wananchi katika mataifa mengine.
“Kwa hiyo ninachukua fursa hii kuwasalimu ndugu zetu wa India katika siku hii muhimu na adhimu na kuwatakia maendeleo zaidi siku zijazo huku tukitarajia kuongeza kasi ya ushirikiano kati ya nchi zetu na watu wake,” alisema.
Wakati huo huo Dk. Shein, amemtumia salamu za pongezi Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi kwa kuadhimisha miaka 68 ya uhuru wa India .
Katika salamu zake hizo Dk. Shein alisema yeye binafsi na wananchi wa Zanzibar wanayo furaha kuungana na Narendra na ndugu zao wananchi wa India katika kusherehekea siku ya uhuru wa nchi hiyo.
Alitumia fursa hiyo kumtakia afya njema na maisha marefu Waziri Mkuu huyo.