Na Mwandishi wetu
James Gashumba, EANA
BENKI zilizomo katika nchi wananchama za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zinatarajia kukua na kupanuka katika kipindi cha miaka miwili ijayo, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na taasisi huru yenye makao yake makuu nchini Marekani.
Kubwa la kuzifikisha benki hizo katika hatua hiyo ya matumaini ni pamoja na kukua kwa pato la taifa kwa mwaka (GDP) kwa kila nchi mwanacahama wa EAC, ripoti iliyotolewa wiki iliyopita ilifafanua.
Ripoti hiyo ijulikanayo kama “Jumuiya ya Afrika Mashariki: Masuala ya mikopo kwa benki” iliyofanyiwa utafiti na taasisi moja ya Marekani ya Moody Investment Services, inaonyesha kwamba sekta ya fedha itakua kwa asilimia 15 katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Taasisi hiyo imekuwa ikitambulika kama ndiyo taasisi ya kitaifa ya masuala ya takwimu (NRSRO) na mashirika ya hisa nchini Marekani.
“Tunaona msukumo mkubwa wa kukua na kupanuka kwa sekta hiyo unatokana na kukua kwa GDP, ukuaji endelevu wa mtangamano wa kanda na kuongezeka kwa idadi ya benki kwa kile kinachoitwa ‘mapinduzi ya huduma za benki za kutembea’' utawarahisishia wateja wengi kufapata huduma za kibenki kupitia simu zao za vikanjani,” alisema Makamu wa Rais wa taasisi ya Moody na Ofisa Mwandamizi wa mikopo, Constantinos Kypreos katika taarifa yake.
Kwa mujibu wa Kypreos, ukuaji mkubwa utaonekana katika benki za Kenya kutokana na ufanisi wa mtandao unaovuka mipaka yake na hali bora zaidi ya teknolojia ya huduma za kutembea za kibenki.
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limekadiria ukuaji wa GDP katika nchi za EAC kuongezeka kutoka kiasi cha asilimia 6.6 mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 6.7 mwaka 2015.
Hali hiyo itasaidia kupanuka kwa huduma za benki kupitia fursa zaidi za biashara na upatikanaji wa mikopo na mahitaji yake.