Na Laylat Khalfan
KAMISHENI ya Utalii Zanzibar, imefanya zoezi la kuzichunguza hoteli zote za Unguja na Pemba pamoja na kuzipandisha daraja zilizostahili ambapo jumla ya hoteli 74 za kitalii zimepandishwa daraja kuanzia la pili hadi la tano.
Afisa anaeshughulikia viwango vya mahoteli Zanzibar , Hassan Burhan wakati akizungumza na Mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Amani Wilaya ya Mgharibi Unguja alisema zoezi hilo lilikagua hoteli 106 kwa hatua ya awali.
Alisema kati ya hizo 74 zilipandishwa daraja tano miongoni mwao 70 kutoka Unguja na 4 Pemba ambapo upandishwaji wa madaraja hayo ulikwenda kwa mujibu wa vigezo vya Afrika Mashariki.
Aidha alisema zoezi hilo litakuwa endelevu na linalenga kubadili mwonekano wa awali wa hoteli kulingana na mahitaji ya ulimwengu ili kumudu ushindani wa biashara na kuiwezesha Zanzibar kupokea wageni wa daraja la juu katika kufaidika na sekta ya utalii.
Alisema miundombinu mibovu kwa baadhi ya hoteli za kitalii imekuwa ikikimbiza watalii matajiri nchini kutona na kukosekana kwa viwango vinavyostahili, jambo linalorudisha nyuma ongezeko la pato la nchi.
Akitaja vigezo vilivyozingatiwa ni pamoja na ubora wa majengo, kuwepo kwa huduma ya usalama na uhifadhi wa mizigo kwa wageni, vifaa vya kuwahudumia ikiwemo vyakula na lugha nzuri.
Alifahamisha hoteli yenye viwango zitatoa huduma ya vyeti maalum vitavyosaidia kujitangaza na kupata wageni kufuatia huduma bora wanazozitoa sambamba na hilo alihimiza umuhimu wa wamiliki wa hoteli hizo kufuata mfumo wa kisasa ili kufaidika na sekta ya utalii wa daraja la juu kama ilivyo kwa nchi nyengine za Afrika mashariki.