Na Mwanrafia Kombo, MCC
VIONGOZI wa jimbo la Makunduchi wametakiwa kubuni miradi ya maendeleo, licha ya kuwepo kwa mafanikio makubwa jimboni humo ikiwemo kupatiwa ufumbuzi kwa tatizo la maji safi na salama.
Wito huo ulitolewa na Mwakilishi wa jimbo la Makunduchi, Mhe. Haroun Ali Suleiman wakati akizungumza na masheha wa shehia za Makunduchi.
Alisema miradi ya maendeleo bado inahitajika katika jimbo hilo ili kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayowakabili wananchi wa jimbo hilo .
Aliwataka wananchi jimboni humo kuendelea kuitunza miradi waliyonayo ikiwemo ya maji safi na salama ili kutufaika kwa mda mrefu.
Mhe. Haroun alieleza endapo kutakuwa na miradi ya uhakika na kuendelezwa kama ilivyokusudiwa, itaweza kumaliza matatizo yanayowakabili wananchi hao sambamba na jimbo hilo kupiga hatua kimaendeleo.
Kwa upande wao Masheha wa shehiya hizo walisema watakuwa mstari wa mbele kusimamia na kuendeleza miradi hiyo ili kuhakikisha wanaondokana na tatizo la utegemezi.
Nae Afisa wa Mamlaka ya maji Zanzibar (ZAWA), Nd. Zahor Suleiman alielezea kuwa sehemu nyingi za Makunduchi zimeshapatiwa ufumbuzi wa tatizo la maji safi na salama na kuongeza kuwa ni maeneo machache ambayo yanatarajiwa kukamilisha si muda mrefu.