Na Khamis Amani
KESI inayowakabili Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Oamar Makame na Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) Salum Msangi, waliofunguliwa mashtaka na ndugu wa watu wanane kwa kuwashikilia kwa muda mrefu bila kuwafikisha mahakamani, limepigwa kalenda hadi Agosti 19 mwaka huu.
Kesi hiyo inasikiliwa na Jaji wa mahakama kuu Zanzibar, Mkusa Issack Sepetu.
Naibu Mrajisi wa mahakama kuu, Yessaya Kayange, aliiahirisha kesi hiyo jana baada ya Jaji anaeisikiliza kutofika mahakamani na sasa itafikishwa tena mahakamani Agosti 19 kwa ajili ya kutajwa.
Ombi hilo liliwasilishwa mahakamani hapo na familia ya watu hao kupitia Wakili wa kujitegemea Abdallah Juma na Rajab Abdalla kutoka Kampuni ya AJM & Solicitor Chamber ili kuielezea mahakama mahali walipo ndugu zao.
Hatua hiyo imekuja baada ya jamaa hao wa karibu wa watu hao kuwatafuta kwa muda mrefu bila ya matumaini ya kuwaona licha ya jeshi la polisi kukiri kuwashikilia.
Watu hao walikamatwa katika maeneo tafauti ya mji wa Zanzibar na jamaa hao hawawajui mahali walipo licha ya juhudi za kuwasaka maeneo tafauti ikiwemo na vituo vya polisi kushindikana.
Kutokana na hali hiyo, jamaa hao walilazimika kuwafikisha mahakamani maofisa hao wakuu wa polisi ili kuelezea mahali walipo.
Kwa mara ya kwanza kesi hiyo ilianza kusikilizwa Julai 21 lakini upande wa polisi ulikiri kwamba unawashikilia na wameshafikishwa mahamani Kisutu.
Hata hivyo, siku nyengine iliyopangiwa kusikilizwa Julai 24, Jaji Mkusa aliifuta kwa kuwa hati ya kiapo haikuwa na saini ya Mrajisi.
Hata hivyo, upande wa walalamikaji hawakuridhika na uamuzi wa mahakama kuu na kuamua kuirejesha tena kesi hiyo mahakamani Agositi 11.
Watu hao waliodaiwa kukamatwa ni Nassor Ahmad Abdallah, Mohammed Is-haq Yussuf, Said Kassim Ali, Hassan Bakari Suleiman, Rashid Ali Nyange, Antar Humoud, Khamis Salum Amour pamoja na Salum Ali Salum.