Na Mwashamba Juma
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Mhe. Juma Duni Haji, ameahidi kuzifanyia kazi changamoto muhimu zinazoukabili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar.
Alisema uwanja huo umekuwa na mahitaji makubwa ikilinganishwa na uwezo wake wa kutoa huduma, hivyo unahitaji kuboreshwa ili kijitosheleza na utoaji wa huduma bora kwa wasafiri ili hadi yake ilingane na viwanja vyengine vya kimataifa.
Aliyasema hayo jana wakati wa ziara yake ya kutembelea Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar,kufua uteuzi mpya uliofanwa na Rais wa Zanzibar hivi karibuni.
Alisema atashirikiana na viongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege pamoja na watendaji wa Wizara yake, kuishauri serikali kuongeza iadadi ya wawekezaji katika uwanja huoo ili kukidhi haja ya kuwepo huduma zenye ubora kwa abiria.
“Biashara ni huduma, wasafiri wanahitaji huduma wanazostahili pamoja na kauli njema ili wafarijike,pia tuwape moyo kwa kuziboresha haraka iwezekanavyo ili wasivunjike moyo,” alisema.
Alieleza uwanja wa ndege na bandari ni uso na taswira ya nchi hasa kwa wageni wanaofika kwa mara ya kwanza nchini.
Alisema haiba njema ya maeneo hayo zitawavutia wageni kuwa na hamu ya kurejea tena nchini kwa ajili ya matembezi pamoja na kuitangaza nchi kimataifa.
Akizungumzia usalama kwa wenyeji na wageni wanaotumia uwanja huo, alipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kwa kutekeleza kwa kivitendo sheria za kimataifa za kutenganisha baina ya wasafiri wa kimataifa na wa ndani ili kupunguza msongamano.
“Dunia imeharibika kila mmoja ana hasira zake, hatuwezi kuziba miaya ya watu kwa asilimia mia moja, lakini kwa kushirikiana tuchukue tahadhari mapema,” alsiema.
Kuhusu tatizo la gari la zima moto katika viwanja hivyo, alisema mamlaka inafanyakazi na jumuiya za kimataifa hivyo suala la zima moto ni muhimu kwa maeneo kama uwanja wa ndege na kuongeza linahitaji ufumbuzi wa haraka.
Aliwataka wafanyakazi wa wizara hiyo kumpa ushirikiano katika kutenganeza na kufanikisha malengo ya wiraza kwa kuhakikisha wanakuwa wakweli na wawazi.
Akitoa ufafanuzi kuhusu maradhi ya Ebola, Ofisa kutoka mamlaka hiyo, Zaina Ibrahim, alisema mamlaka imejipanga kukabiliana kwa namna yoyote na ugonjwa huo ili usiingie nchini.
Alisema mamlaka ina utaratibu wa kukutana na watendaji wa kitengo cha huduma cha uwanja wa ndege ili kufanikisha mikakati waliojiweke.
“Awali tuliweka mikakati ya kujikinga wenyewe pamoja na kuwakagua abiria ili kuwatambua wenye maradhi kwa kutumia kifaa maalum, kusajili wageni wote wanaoingia nchini ili kuwajua sehemu wanazotoka pamoja na kujua maeneo na muda watakaokaa nchini kwa kueneza fomu zao wilaya zote na tunawafuatilia muda wote,” alisema.
Alisema hatua nyengine endapo watagundua kama kuna ndege imeingia nchini na ina mgonjwa wa Ebola, wataitenga mbali na watu ndege hiyo.
Awali akizungumzia changamoto,Mkurugenzi rasilimali watu wa mamlaka hiyo, Muhidini Talib Abdallah, alisema miongoni mwao ni kutokukabilika kwa ujenzi wa eneo la abiria wa ndani wakati huduma zinaendelea, abiria kupata jua na mvua kutoka eneo la maegesho ya ndege hadi jengoni, msongamano wa wageni wanaoingia na kutoka nchini pamoja na utaratibu wa kuwahudumia wagonjwa na wanaohitaji msaada.