Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Makamba:Kampuni za simu zinawaibia wateja

$
0
0
Na Fatina Mathias, Dodoma
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, amekiri kuwepo tatizo la wizi wa fedha za Watanzania unaofanywa na kampuni za simu za mikononi, ambazo zinawakata wateja fedha zao kiholela.

Kauli hiyo aliitoa jana bungeni mjini hapa alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji, aliyetaka kujua ni nani aliyeko nyuma ya pazia huku serikali makini ya CCM ikikaa kimya bila kuchukua hatua na kuacha mamilioni ya Watanzania yakiibiwa na kampuni za simu.

Alisema kumekuwepo na tatizo hilo na kwamba ni kubwa ambapo katika kulidhibiti wameweka kanuni na taratibu za kudhibiti vitendo hivyo.

“Ni kweli kabisa Watanzania waliko vijijini ambao ndio wengi hawana uwezo wa kumudu gharama za kusafiri hadi Dar es Salaam kwenye makao makuu ya kampuni ya simu kwa ajili ya kudai fedha hizo wanazokatwa na pia serikali ilibaini kuwepo tatizo la kampuni za simu kuwa na utaratibu wa kupuuza wateja na kuchelewa kufanyia kazi malalamiko ya wateja,”alisema.


Alisema baada ya kulibaini hilo waliamua kutoa utaratibu wa kawaida wa wateja kulalamika kwenye kampuni za simu.
“Wateja wamekuwa wakipata shida kwani hata wapopiga simu kwa ajili ya kulalamika hujikuta wakikatwa tena fedha zao hivyo kama serikali tunalitambua suala hili,”alisema.

Hata hivyo, alisema wameweka mtambo maalum  wa kufuatilia mawasiliano ambayo kazi moja wapo ni kufuatilia mapato, kuimarisha huduma za mawasiliano na kutakuwa na namba za bure ambazo zitasambazwa kwa Watanzania kwa ajili ya kupiga na kutoa malalamiko yao ambapo kila lalamiko litapewa namba maalumu.

Aidha alikanusha vikali CCM kuhusika na wizi wa fedha za Watanzania kwa njia ya mitandao unaotokana  na kampuni ya simu.

Akijibu swali la msingi, Makamba alisema Serikali kwa kutambua umuhimu wa kulinda haki za walaji wa huduma za mawasiliano, mwaka 2011 ilitunga kanuni za kulinda walaji ambazo zinabainisha haki na wajibu wa watumiaji wa huduma hizo.

Alibainisha pale ambapo itathibitishwa kwamba kampuni ya simu imekiuka masharti ya mkataba na leseni ya huduma kwa wateja, kampuni husika hupaswa kumlipa fidia mteja wake.


Aliwaasa watumiaji wa huduma za mawasiliano wawe wanawasilisha malalamiko katika ngazi husika kama sheria na kanuni zinavyoagiza.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>