DARFUR, Sudan
WANAJESHI wanne wa kulinda amani wa Umoja katika eneo la Darfur nchini Sudan hawajulikani waliko baada ya kusombwa na maji ya mafuriko.Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa, Rania AbdulRahman, amesema wanajeshi hao walikuwa wakisindikiza msafara wa magari ya kutoa misaada, wakati waliposombwa na maji.
Afisa huyo alisema kuwa wanajeshi wengine wawili walipatikana wakiwa hai na kundi la uokoaji.
Umoja wa Mataifa haujatoa majina au uraia wa wanajeshi hao ambao hawajulikani waliko.
Mwezi Agosti mwaka uliopita wanajeshi watatu kutoka Tanzania walizama majini baada ya gari lao la kijeshi, kukwama katika mto mmoja nchini Sudan.
Wanajeshi hao walikuwa wakielekea eneo la Misterei, takriban kilomita 50 kusini magharibi mwa mji mkuu wa eneo hilo Geneina wakisindikiza msafara wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani ,WFP, wakati msafara wao uliposombwa na mafuriko.
Kikosi cha kulinda amani nchini Sudan kinakabiliwa na upungufu wa vifaa vya kutosha na vya kisasa, hali ambayo inaadhiri juhudi zao za kutunza amani katika eneo hilo la Darfur.
Wanajeshi hao wa Umoja wa Mataifa, wako katika eneo hilo la Darfur, kujaribu kumaliza mzozo uliodumu kwa miongo kadhaa kati ya wanajeshi wa serikali na waasi.
Hivi karibuni Tanzania ilipoteza wanajeshi wake saba katika jimbo la Darfur baada ya kushambuliwa na waasi.
Shirika la Afya Duniani,WHO, limesema kuwa zaidi ya watu laki tatu nchini Sudan, wameathiriwa na mafuriko na zaidi ya watu 50 wamefariki mwezi huu.
Shirika hilo limesema kuwa eneo linalokaribia mji mkuu wa Khartoum ndilo limeathirika zaidi na mafuriko hayo ambayo ndiyo mabaya zaidi kuwahi kukumba eneo hilo kwa zaidi ya miaka ishirini na mitano iliyopita.
Msemaji wa WFP, Amor Almagro amethibitisha kuwa wafanyakazi wa shirika hilo waliokuwa kwenye msafara huo, watano kati yao raia wa Sudan na wawili wa mataifa ya kigeni wako salama.