Na Mwantanga Ame, Dodoma
KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imebatilisha uamuzi uliofanywa na Halmashauri Kuu CCM ya Mkoa wa Kagera wa kuwafukuza uanachama Madiwani wanane wa chama hicho. Taarifa iliyotolewa na Katibu wa NEC Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye imesema Madiwani hao wanane ni wanachama halali wa CCM.
Alisema Kamati Kuu imetoa uamuzi huo, baada ya kubaini kuwa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera haikuzingatia katiba ya CCM ya 1977 toleo la 2012 ibara ya 93 (15).
“Kumwachisha au kumfukuza uongozi kiongozi yeyote ambaye uteuzi wake wa mwisho unafanywa na Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa, isipokuwa kwa suala la kumvua uanachama au uongozi Diwani lisifanyike hadi Kamati Kuu imearifiwa na kutoa maelekezo,” alisema.
Aidha, Kamati Kuu imewaonya Madiwani wa CCM wa manispaa ya Bukoba, Mbunge wa Bukoba Mjini na Meya kwa kusababisha kukosekana utulivu, mshikamano na amani katika manispaa na chama.
Kamati Kuu pia imeitaka serikali kumwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum wa haraka wa mambo yanayolalamikiwa dhidi ya Meya ili ukweli ujulikane na matokeo ya uchunguzi huo yawasilishwe kwenye baraza la madiwani ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazoongoza serikali za mitaa.
Alisema wakati tuhuma hizo dhidi ya Meya zikichunguzwa, Kamati Kuu imewataka Madiwani wa CCM kurejesha utulivu kwenye manispaa na chama kwa ujumla ili kufanikisha utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM na kuwaletea maendeleo wananchi wa Bukoba.