Na Khamis Choum na Mwantanga Abdallah, ZJMMC
SHIRIKA la Biashara Zanzibar (ZSTC) linatarajia kutumia kiasi cha shilingi bilioni 32.5 kununua karafuu kavu kutoka kwa wakulima msimu huu wa mavuno.Kauli hiyo imetolewa na Naibu Mkurugenzi wa Shirika hilo, Suleiman Juma Jongo, alipozungumza na waandishi wa habari hizi ofisini kwake Maisara kuhusu zoezi la uchumaji na ununuzi wa karafuu linaloendelea.
Alisema kwa mwaka huu wanatarajia kununua zaidi ya tani 4,852 za karafuu kavu.
Aidha alisema wanatarajia kujenga vituo vitano vya ununuzi wa karafuu kwa kila msimu Unguja na Pemba sambamba na kuvifanyia marekebisho vituo vya Shungi, Uondwe, Chimba, Mgogoni na Pangani kisiwani Pemba.
Alisema kutokana na uzalishaji mkubwa unaoendelea kisiwani Pemba, mkakati zaidi utawekwa huko huku juhudi za kuimarisha uzalishaji karafuu kisiwani Unguja zikiendelea.
"Msimu huu tunatarajia kujenga vituo vitano katika maeneo ya Chanjaani, Gando, Bwagamoyo kwa wilaya ya Wete, Chambani na Wambaa kwa wilaya ya mkoani Pemba,” alisema.
Alifahamisha kuwa katika kurudisha kasi na hadhi ya zao la karafuu visiwani humo, wataendelea kuwaongezea bei wakulima sambamba na kuvipa motisha vikundi vya wakulima vilivyokaa pamoja na kuotesha miche ya mikarafuu.
Akizungumzia kuhusu kupambana na wanaosafirisha karafuu kwa njia ya magendo, alisema wameanzisha kitengo maalumu cha kupambana na biashara hiyo ambacho kinajumuisha wakuu wote wa vikosi vya ulinzi na usalama, wakuu wa mikoa na wilaya na viongozi wa shirika hilo.
Aliwahimiza wananchi kuziuza karafuu zao katika shirika la ZSTC na kuacha kushawishika kuuza karafuu kwa njia ya magendo.