Na Abdi Suleiman, Pemba
MTU mmoja amefariki dunia na wengine 19 wamejeruhiwa, akiwemo mtoto mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu, baada ya gari ya abiria waliyokuwa wakisafiria kutokea Wesha kwenda Chake Chake, kupinduka katika eneo la Kichanjaani Ndagoni mkoa wa kusini Pemba.
Akithibitisha tuko hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Saleh Mohamed Saleh, alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 12:55 asubuhi, wakati gari hiyo ilipokuwa ikipanda mlima.
Alimtaja marehemu kuwa ni, Ibrahim Mbarouk Seif (18), mkaazi wa Kichanjaani Ndagoni, na majeruhi wamkimbizwa hospitali ya Chake Chake kwa matibabu.
Aidha aliitaja gari iliyopata ajali kuwa ni Z124 BT yenye ruti 305 Wesha-Chake, iliyokuwa ikitokea Kichanjaani Ndagoni na kuelekea mjini, huku dereva na utingo wa gari hizo wakishikiliwa kwa maelezo zaidi.
Alimtaja dereva wa gari hiyo kuwa ni Salim Kassim Usi (30) na utingo Juma Khamis Kombo (20) wakaazi wa Buyuni Wesha, huku majeruhi watatu wakiwa wamelazwa hospitalini.
Kwa upande wake daktari dhamana wa hospitali ya Chake Chake, Yussuf Hamad alisema marehemu alifariki baada ya kuvunjika mbavu tatu za mkono wa kulia hali iliyopelekea mapafu yake kutokufanya kazi zake vizuri.
Dk Yussuf aliitaja sababu nyengine iliyopelekea kifo cha marehemu huyo, kuwa ni kuumia sehemu za kichwa.
Waliojeruhiwa ni Salum Nassor Khamis (20), Habiba Khamis Shaib (8), Mohamed Ali Hamza (12), Rabia Yahya Salim (18), Maruwa Haji Hamad mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu, Asha Hamad Mohamed (35).
Wengine ni Abdi Hamza Khamis (47), Mafunda Omar Rashid (49), Yakub Asaa Abdalla (9), Hamad Khamis Rashid (12), Salim Omar Said (24), Kame Abuu Kai (17), Shafi Maktuba Kahatan (20), Mwamvua Kombo Iddi (25), Suleiman Khamis Said (18), Omar Hemed Sharif (29), Fatma Ali Mohamed (30), Atie Rashid Omar (3) na Omar Rashid Omar.