Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Oman Zanzibar Kushirikiana Sekta ya Habari.

$
0
0
Na Mwandishi wetu
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Ufalme wa Oman, zimeahidi kushirikiana katika sekta ya habari wa faida ya wananchi wan chi mbili hizo.

Ahadi hiyo imetolewa na Mawaziri wa habari wan chi hizo walipokutana ukumbi wa VIP hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar wiki iliyopita.

Akizungumza katika hafla ya chakula cha jioni ambayo Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar imeandaa kwa ujumbe wa Serikali ya Oman ulioongozwa na Waziri wa Habari wa Oman, Dk. Abdulmonam Mansoor Al-Hasani, waziri wa Habari wa Zanzibar, Said Ali Mbarouk, alisema kwamba kuna kila sababu ya Zanzibar na Oman kushirikiana kwa faida za watu wao ambao wana historia ya udugu ya muda mrefu.

Waziri Mbarouk alisema kwamba viongozi wa Serikali ya Zanzibar wanapokutana na viongozi wa Serikali ya Oman, kama ilivyo kwa watu wa nchi hizo mbili huwa hawazungumzi kama mwenyeji na mgeni bali kama ndugu kutokana na uhusiano wao kihistoria na kidamu.

Waziri Mbarouk aliyeambatana na Watendaji wakuu wa taasisi za habari zilizo katika Wizara yake, aliueleza ujumbe wa Oman mafanikio na changamoto zinazovikabili vyombo vya habari Zanzibar, pamoja na sekta hiyo muhimu kwa jumla.

Aidha waziri Mbarouk alieleza maeneo ambayo nchi mbili hizo zinaweza kushirikiana ikiwemo kubadilishana habari, utaalamu, vifaa na mambo mengine, ikiwemo teknolojia ya digitali ambayo Oman imeshapiga hatua kubwa wakati Zanzibar ndio imeanza karibuni.

Nae waziri wa Habari wa Oman, Dk. Abdulmonam, alisema mbali ya maeneo hayo ambayo yameelezwa na waziri Mbarouk, Oman na Zanzibar zinaweza kushirikiana katika maeneo mengi zaidi katika sekta ya habari.

Dk.Abdulmonam alisema yeye na ujumbe wake wamefarajika na ukarimu waliooneshwa na Serikali na wananchi wa Zanzibar kwa kipindi chote walichokuwepo Zanzibar wakihudhuria Kongamano la kimataifa la Utafiti wa historia ya Ustaarabu wa kiislamu kwa nchi za Afrika Mashariki lililofanyika hoteli ya Lagema Zanzibar wiki iliyopita.

Katika hafla hiyo ya chakula cha jioni, Waziri Dk. Abdulmonam aliongozana na viongozi mbali mbali kutoka Oman akiwemo Katibu wa Mufti wa Oman, pamoja na Balozi wa Oman nchini Tanzania, Yahya Moosa Albakri na Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar, Salleh Suleiman Al-Harith.

Pamoja na waziri Mbarouk kwa upande wa Zanzibar pia alikuwepo waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakary, Naibu waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Bihindi Hamad Khamis, Katibu Mkuu Wizara hiyo, Dk.Ali Mwinyikai na Naibu Katibu Mkuu, Issa Mlingoti.

Wengine ni Watendaji wakuu wa Shirika la Magazeti ya Serikali linalochapisha magazeti ya ‘Zanzibar Leo’, ‘Zanzibar Leo Jumapili’ na ‘Zaspoti’, Mkurugenzi Mkuu na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), Mkuu wa Chuo cha Uandishi wa habari cha Zanzibar na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar na watendaji wengine wa Wizara hiyo.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>