Na Kadama Malunde,Kahama
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja amesema Watanzania wanakumbuka na wataendelea kumkumbuka Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowasa na kwamba sio mtu mdini,mkabila wala mtu wa kundi lolote bali ni mtu mpole, mwaminifu, mtanashati anayejali maendeleo ya Watanzania.
Mgeja aliyasema hayo katika viwanja vya kanisa la AICT Pastoreti ya Kahama mjini wakati wa harambee ya ujenzi wa shule ya msingi itakayoitwa Neema AICT Kahama mjini ya kanisa hilo ambapo mgeni rasmi alikuwa Lowasa.
Alisema mchango wa Lowasa katika taifa utaendelea kukumbukwa hasa katika sekta ya elimu na maji tangu akiwa Waziri wa Maji na baadae Waziri Mkuu.
“Tunakumbuka na tutaendelea kukumbuka mchango wa ndugu yetu Lowasa,katika suala la elimu,huwezi achanisha shule za sekondari za kata na Lowasa,shule hizo ni msingi wa Lowasa na serikali inaziendeleza na ana mchango mkubwa pia katika sekta ya maji na sasa wananchi wa mkoa wa Shinyanga tayari wanatumia maji kutoka ziwa Victoria na yanapelekwa pia mkoani Tabora,” alisema.
Mgeja aliwataka Watanzania kuwapuuza baadhi ya watu wanaomchafua Lowasa na kuongeza kuwa watu hao watashindwa kwa jina la Yesu huku akimwomba Lowasa kuwa na subira na kuwapuuza watu hao wenye chuki na kuongeza kuwa Lowasa ni kama mto Ruvu ambapo huwezi zuia maji yake kwa mikono.
“Ndugu yangu Lowasa,sifa zako nzuri ndizo zinakugharimu,lakini wanaokuchafua wanahangaika na kivuli chako!,hawawezi kukukwamisha,wala wasikukatishe tamaa,fanya kazi uliyotumwa na Mungu wetu,kwani hata mti wenye matunda mazuri ndio hupigwa mawe,huwezi kukuta watoto wanapopoa mawe mkaratusi,” alisema.
Akizungumza katika harambee hiyo Lowasa alisema yeye hana nia ya kuwajibu wanaomchafua kwani lengo lake ni kuwaletea maendeleo wananchi na wala sio kujibishana na mtu yeyote.
"Sina nia ya kuwajibu wanaonichafua,najua mtetezi wangu ni mungu,niko imara,sitetereki na wanaonichafua,nitaendelea kuwasaidia wananchi kadri niwezavyo, jambo jingine nawaomba nyie wazazi na walezi jengeni msingi mzuri kwa watoto wenu kwa kuwapeleka shule na kuwa na moyo wa kuchangia katika shughuli na miradi mbalimbali ya maendeleo”, alisema.
Awali Askofu wa kanisa AICT dayosisi ya Shinyanga, John Nkola alisema shule hiyo ya msingi itasimamiwa na kanisa la AICT pastoreti ya Kahama mjini lenye waumini zaidi ya 500 na itatumiwa na watoto kutoka maeneo mbalimbali nchini bila ubaguzi.
Katika harambee hiyo zaidi ya shilingi milioni 212 zilipatikana ambapo malengo yalikuwa kukusanya shilingi milioni 150.