Na Hafsa Golo
SERIKALI imewaagiza wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu jua kali waliopo Darajani kuondoka na kurejea Saateni bila mivutano.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum, Haji Omar Kheir wakati akizungumza na vyombo vya habari jana.
Alisema muda waliopewa wa kubakia katika eneo hilo umemalizika hivyo vi vyema kufuata taratibu na makubaliano ili kuondoa usumbufu usio wa lazima.
Alisema lengo la serikali ni kujenga mazingira yaliyo bora katika eneo hilo hasa ikizingatiwa eneo hilo ndio kitovu cha mji huo, na kamwe haina nia ya kuwatesa wananchi wake.
Alisema watafanya juhudi ya kutoa miongozo kwa njia ya busara na wana matumaini kwamba wafanyabiashara watatekeleza ipasavyo agizo hilo na kwa wale ambao watakaidi itabidi walazimishwe kuondoka.
Alisema baada ya kuteuliwa kuongoza wizara hiyo alitembelea manispaa ya mji wa Unguja na Halmashauri ya wilaya ya magharibi na kubaini changamoto mbali mbali ikiwemo watu kutotii sheria,kufanya biashara holela, tatizo la usafi na ulipaji wa ada.
Alisema wizara itahakikisha pamoja na wafanyabiashara hao kuwapatia elimu na taratibu za kimsingi.
Aliwataka wananchi kushirikiana na baraza la manispaa,mabaraza ya miji na halmashauri kutunza mazingira yaliowazunguka ili kuweka mji katika hali ya safi.