Na Kija Elias, Moshi
JESHI la Polisi linawashikiliwa watuhumiwa wengine wanne akiwemo mfanyabiashara wa madini ya tanzanite jijini Arusha, Joseph Damas maarufu Chusa kuhusiana na mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Erasto Msuya (43) aliyeuawa hivi karibuni kwa kupigwa risasi.
Watuhumiwa hao, Jalila Zuberi Said (28), mkazi wa Babati, lakini pia anakaa Manyara na Kondoa, Sadiki Mohammed Jabir (32), mkazi wa Dar es
Salaam na Langata wilayani Hai na Karim Kihundwa (33) mkazi wa kijiji cha Lawate wilayani Siha wanatarajiwa kuunganishwa katika kesi hiyo inayosikilizwa katika mahakama ya hakimu mkazi Moshi mkoani Kilimanjaro.
Watuhumiwa hao walikamatwa, Septemba 13 mwaka huu, ambapo kwa mujibu wa taarifa kutoka Polisi mkoani Kilimanjaro zilizotolewa na Kamanda,Robert Boaz watuhumiwa wawili, Sadiki Mohamed na Karim Kihundwa walikamtwa Sikonge mkoani Tabora wakielekea kwa mganga wa jadi.
Kamanda Boaz alisema baada ya kukamatwa watuhumiwa hao, jeshi la polisi liliwahoji na kuwaonesha polisi silaha namba KJ 10520 iliyotumika katika mauaji hayo pamoja na pikipiki yenye namba za usajili T751 CKB.
“Tulifanikiwa kuwakamata na katika mahojiano yetu tulibaini silaha iliyotumika namba KJ 10520 pamoja na pikipiki namba za usajili T751 CKB, alisema.
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao imekuja baada ya watuhumiwa wengine watatu, Sharifu Athumani Mohammed (31), mkazi wa Kimandolu, jijini Arusha, Shaibu Mredi Mpungi (38), mkazi wa kijiji cha Songambele, wilaya ya Mererani, mkoani Manyara na Musa Mangu (38), mkazi wa
Shangarai kwa Mrefu, jijini Arusha,kutiwa mbaroni kuhusiana na mauaji hayo na kufikishwa mahakamani, Agosti 21 mwaka huu.
Msuya aliuawa Agosti 7 mwaka huu majira ya 6:30 mchana kwa kupigwa risasi kando ya barabara kuu ya Arusha - Moshi katika eneo la Mjohoroni, wilaya ya Hai, karibu na uwanja wa ddege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Septemba 18, mwaka huu.