Na Mwandishi maalum, New York
RAIS wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete amezungumza kwa simu na mwenzake wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta kufuatia shambulizi la kigaidi katika duka la kifahari Westgate mjini Nairobi.Akiwa mjini New York anakohudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais Kikwete alimwambia Rais Kenyatta kwamba Tanzania inaungana na ndugu zao wa Kenya katika msiba huo mkubwa.
Rais Kikwete aliliita shambulizi hilo kuwa baya na kusema Tanzania itaendelea kushirikiana na Kenya kukabiliana na ugaidi.
Shambulizi hilo la kigaidi lililotekelezwa na wanamgambo wa Al Shabaab limesababisha vifo vya watu 68 huku wengine zaidi ya 170 wakijeruhiwa.
Alisema Tanzania inachukua tahadhari kuhakikisha mashambulizi hayo hayatokei ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi wa mipakani.
Rais Kikwete walimuomba Mwenyezi Mungu kuziweka pema roho za watu waliopoteza maisha katika shambulizi hilo na kuwaombea nafuu ya haraka majeruhi.