Na Kadama Malunde, Shinyanga
ASKARI Polisi watatu wamekufa papo hapo na wengine wanane kujeruhiwa wakiwemo maafisa wawili wa Idara ya Uhamiaji kufuatia gari walilokuwa wakisafiria kupinduka.Ajali hiyo ililihusisha gari lenye namba za usajili PT 0762 aina ya Randrover mali ya jeshi la polisi mkoa wa Njombe.
Ajali hiyo ilitokea juzi majira ya saa 12:00 jioni katika kijiji cha Malenge kata ya Kagongwa wilayani Kahama wakati askari hao wakitokea mkoani Kagera kurudi mkoani Njombe baada ya kumaliza operesheni ya kuwasaka wahamiahi haramu maaru operesheni kimbunga.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Kihenya Kihenya aliwataja askari waliofariki kuwa ni Koplo Fred, (32) ambaye anafanya kazi kituo cha Makambako Mbeya, PC Sufian (28) anaefanya kazi Makambako na PC Maiko (27) askari polisi kutoka kituo cha Njombe.
Alisema maiti za askari hao zimehifadhiwa hospitali ya wilaya ya Kahama mkoani hapa huku akiwataja waliojeruhiwa kuwa ni Mkaguzi Reonard ambaye aliumia sehemu ya kiuno, PC Yusuph (32) kutoka kituo cha Njombe ambaye alikuwa dereva,PC Lambard(30), PC Hussein,PC James (23) na PC Adam (28).
Alisema katika ajali hiyo walikuwepo maafisa uhamiaji wawili ambao pia walijeruhiwa.
Maafisa hao ni Agustino Nanyambe (31) kutoka makao makuu ya uhamiaji mkoa wa Rukwa na Glory Temu kutoka Mbeya.
Alisema chanzo cha ajali hiyo kinachunguzwa na majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Kahama.