Na Mwandishi Wetu
MKE wa Rais wa Zanzibar, Mama Mwanamwema Shein, amewataka Vijana wa Chama cha Mapinduzi, kuibua mambo mapya ya maendeleo yatayoifanya Zanzibar kuwa nchi yenye mafanikio na kukuza soko la ajira kwa vijana.
Mama Shein, aliyasema hayo jana wakati akikabidhi vifaa mbalimbali vya muziki kwa bendi ya Vijana wa Chipukizi wa Chama cha Mapinduzi, huko katika uwanja wa Gombani Wilaya ya Kusini Kisiwani Pemba.
Mama Shein, alisema Chama cha ASP, wakati kinaanzisha kiliona umuhimu wa kuwaunganisha vijana kwa kuweka utaratibu maalum wa kuwaandaa vijana kuwa na uzalendo wa kuipenda nchi yao na kuweza kuwa warithi wa taifa hili hapo baadae.
Alisema ni laziama vijana wathamini jitihada za Chama cha CCM, kwa kuwaandaa ili waweze kukabiliana na soko la ajira pamoja na kuwa na uzalendo wa kuipenda nchi yao .
Alisema utaratibu huo kwa kiasi kikubwa uliweza kusaidia serikali kuweza kupata vijana walio na uzalendo wa nchi yao, pamoja na waaminifu na walinzi shupavu wa nchi yao.
Alisema bila ya kuwaandaa vijana nchi inaweza ikayumba kwani wanahitaji kuona wanaandaliwa kiakili, elimu, kinidhamu, kimaadili na kupewa mafunzo yatayoweza kuwajengea uzalendo.
Alisema serikali inapenda kuona vijana wa Zanzibar, wanakuwa ni wenye uwezo wa kuibua mambo mapya ya kimaendeleo ambayo kwa kiasi kikubwa yataweza kuwafanya kuwa washupavu zaidi katiuka shughuli zao.
Hata hivyo, Mama Shein, aliwataka vijana hao kuona umuhimu wa kuyathamini Mapinduzi ya Zanzibar kwa vile ndio yaliowakomboa vijana kuweza kufanya shughuli zao chini ya Jemedari wa Mapinduzi, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Nae Mke wa Makamu wa Pili wa Rais, Mama Asha Suleiman Iddi, akitoa maelezo yake, alisema vijana nchini wa kila sababu ya kuhakikisha hawayumbishwi katika kukitetea chama chao.
Alisema Chama cha CCM, kimeona umuhimu wa kuwaunganisha vijana na ndio maana kimeamua kuwaundia Umoja wa Vijana.
Kutokana na hali hiyo, Mama Asha, aliwataka kuona haja ya kuwajenga kuwa wamoja iliu waweze kufanya kazi kwa ushirikiano na kuufanya umoja wao kuwa tegemeo kwa vijana wengine.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Shaka Hamdu, amewataka vijana kuona haja ya kutunza amani ya nchi kwa kutambua kwamba uhuru wa nchi haupatikani mara mbili.
Alisema inasikitisha kuona baadhi ya vijana kuingizwa katika vitendo vya vurugu vinavyotokea katika maeneo mbalimbali duniani, jambo ambalo limekuwa likisababisha kupotea kwa uhuru wa nchi zao.
Alisema hali hiyo, imeanza kiuonekana katika mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo Sudani ya Kusini ambapo hivi sasa baadhi ya wananchi wao wamekuwa katika mazingira magumu kutokana na amani kuharibika.
Kutokana na hali hiyo, Shaka alisema viongozi wa Jumuiya hiyo, watahakikisha kuona vijana wanakuwa katika mazingira bora ya maisha yao.
Nao viongozi wa Bendi hiyo, walishukuru kwa msaada walioupata kwa vile utaweza kuifanya bendi hiyo kuendeleza ajira yao.